NBAA YATALIWA KUONGEZA UBUNIFU KATIKA MITAALA ILI KUENDANA NA KASI YA AKILI UNDE
Serikali imeitaka Bodi ya Taifa
ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) kuharakisha maboresho ya mitaala na
mafunzo ya uhasibu ili kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia, hususan
matumizi ya akili unde (AI), kwa kuwa baadhi ya kazi zinazofanywa na wahasibu
hivi sasa zinaweza kubadilika au kutoweka kutokana na mapinduzi hayo ya
kiteknolojia.
Wito huo umetolewa na Naibu
Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), wakati akihutubia kwa niaba ya
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Mahafali ya 49 ya
NBAA yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es
Salaam.
Mhe. Luswetula alisema dunia
inaelekea kwa kasi katika matumizi ya akili unde na kwamba taaluma ya uhasibu
haiwezi kubaki nyuma katika mabadiliko hayo, kwa kuwa inaleta mabadiliko katika
namna kazi mbalimbali zinavyofanyika na kwamba ni muhimu wataalamu wa uhasibu
kuandaliwa mapema ili waweze kutumia teknolojia hiyo kuongeza ufanisi na tija
badala ya kuachwa nyuma na mabadiliko ya kiteknolojia.
“Dunia yote inaelekea kwenye
matumizi ya akili unde, na NBAA pamoja na wadau wengine muangalie mmejipangaje
kukabiliana na mapinduzi haya hasa kuhakikisha mitaala yetu ya mafunzo
imesharekebishwa ili kuendana na mwelekeo wa dunia ya sasa” alisema Mhe.
Luswetula.
Alisisitiza kuwa, Kama Taifa kuna
umuhimu wa kuongeza idadi ya wataalamu wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini
kwa kuzingatia suala la ubora, weledi, uaminifu na uadilifu kama msingi wa
taaluma hiyo, kwa kuwa idadi ya wahasibu wenye sifa bado haitoshelezi mahitaji
yaliyopo katika sekta ya umma na binafsi.
Mhe. Luswetula alisema kuwa
wahasibu na wakaguzi wa hesabu wana nafasi muhimu katika kulinda na kusimamia
rasilimali za Taifa, kwa kuwa taaluma hizo ni miongoni mwa nguzo muhimu za
uchumi, hivyo wataalamu wake wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia
viwango vya juu vya uadilifu na uaminifu.
“Naitaka NBAA kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali kutafuta suluhisho la changamoto ya ukosefu wa mafunzo kwa
vitendo kwa wahitimu wa uhasibu, kwa sababu wahitimu wengi wanapata elimu ya
nadharia darasani zaidi lakini wanakutana na changamoto wanapoingia katika
mazingira halisi ya kazi kutokana na kukosa fursa za kutosha za kujifunza kwa
vitendo” alisema Mhe. Luswetula
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa
karibu na NBAA, ikiwemo kuhakikisha Bodi hiyo inakuwa na watumishi wa kutosha
na wenye weledi unaohitajika huku akiwapongeza wahitimu wa programu mbalimbali
za NBAA, ikiwemo Taaluma ya Juu ya Uhasibu (CPA), Cheti cha Uhasibu (ATEC), CPA
Equivalent, Stashahada ya Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma
(IPSAS), Stashahada ya Kitaalamu katika Ukaguzi wa Ndani (Professional
Diploma in Internal Auditing) na Stashahada ya Kitaalamu katika Utoaji wa
Taarifa za Uendelevu (Professional Diploma in Sustainability Reporting).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa
NBAA, CPA Prof. Sylvia Temu, alisema Bodi hiyo imeendelea kutekeleza majukumu
yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali, huku ikitekeleza
Mpango Mkakati wa Miaka Mitano unaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alisema kupitia mpango huo, NBAA inalenga
kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalamu wa uhasibu waliobobea wasiopungua
90,000 ifikapo mwaka 2050, sambamba na kuimarisha viwango vya taaluma hiyo kwa
kuzingatia viwango vya kimataifa.
“Kipindi cha mwaka 2025/26, NBAA iliendelea
kusimamia mitihani ya kitaaluma, uadilifu wa makampuni yanayofanya shughuli za
kihasibu na ukaguzi wa hesabu, pamoja na kutoa mafunzo endelevu kwa wahasibu,
wakaguzi, watahiniwa, walimu na wadau wengine, na kuendelea kuendana na
mabadiliko ya mazingira ya biashara na uchumi kwa kuwekeza katika maeneo mapya
ya taaluma, ikiwemo masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG)” alisema
CPA. Prof. Temu.
CPA. Prof Temu aliongeza kuwa NBAA imeendelea
kushiriki katika taasisi na majukwaa ya kikanda na kimataifa ya taaluma ya
uhasibu, ikiwemo International Federation of Accountants (IFAC), Pan Africa
Federation of Accountants (PAFA) na Jumuiya ya Professional Accounting Bodies
Afrika Mashariki, hatua inayolenga kuongeza ushindani wa wataalamu wa Tanzania
katika soko la huduma za kitaaluma ndani na nje ya Afrika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya
Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Mzenzi, alisema
kuwa kuanzia mwaka 2022, Bodi hiyo imekuwa ikiendesha mahafali mara mbili kwa
mwaka kwa lengo la kuwawezesha wahitimu kupata vyeti vyao kwa wakati ili waweze
kutumia sifa zao katika kutafuta ajira au kuwasilisha vyeti kwa waajiri wao kwa
ajili ya kupandishwa madaraja.
Aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa
ushirikiano unaoiwezesha NBAA kutekeleza majukumu yake ya kuimarisha taaluma ya
uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini.
“Natoa wito kwa waajiri wa sekta ya umma na binafsi
kutumia wataalamu hawa waliohitimu, na tutaendelea kujenga uwezo katika maeneo
mapya kama alivyoainisha Mgeni Rasmi ili kuongeza idadi ya wataalamu wa maeneo
hayo hususan Sustainability Reporting” alisema CPA Prof. Mzenzi,
Mahafali hayo ya 49 yalihusisha jumla ya wahitimu
681 kutoka katika ngazi saba za taaluma, wakiwemo wahitimu wa Cheti cha
Waandishi na Utunzaji wa Vitabu vya Hesabu (Accounting Technicians), Taaluma ya
Juu ya Uhasibu (CPA), CPA Equivalent, Cheti cha Kitaaluma katika Viwango vya
Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (Professional Certificate in IPSAS),
Stashahada ya Kitaaluma katika Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya
Umma (Professional Diploma in IPSAS), Stashahada ya Kitaaluma katika Ukaguzi wa
Ndani (Professional Diploma in Internal Auditing), pamoja na Stashahada ya
Kitaaluma katika Utoaji wa Taarifa za Uendelevu (Professional Diploma in
Sustainability Reporting).






Post a Comment