PPP-CENTRE: UBIA WA SERIKALI NA SEKTA BINAFSI MUHIMU KUFANIKISHA DIRA YA TAIFA 2050



Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi-PPP-CENTRE, kimesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, kupitia uwekezaji wenye tija na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mkurugenzi Mtendaji wa PPP-CENTRE, David Kafulila, amesema hayo leo mjini Kibaha, mkoani Pwani, wakati akifungua Kongamano la Fursa za Uwekezaji kupitia Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, linalolenga kukuza uwekezaji na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo.

Kafulila amesema ushirikiano huo unatakiwa kuelekezwa katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza ajira na kuchochea ujenzi wa uchumi shindani na endelevu, kwa kuihusisha zaidi sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Richard Kayombo, amesema kongamano hilo ni fursa muhimu ya kuwaelimisha wafanyabiashara na wananchi kuhusu fursa zilizopo za uwekezaji, hatua inayoweza kuchochea ajira na kuongeza kasi ya maendeleo ya Mkoa wa Pwani na Taifa kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Taifa ya Biashara-TNCC, Oscar Kissanga, amesisitiza umuhimu wa kongamano hilo, akisema majukwaa ya aina hiyo husaidia kufungua fursa mpya za uwekezaji, kuwaunganisha wafanyabiashara na wawekezaji, pamoja na kuongeza tija katika sekta binafsi na uchumi wa Taifa.

Kisanga ametoa wito wa kuachana na utaratibu wa “business as usual” katika makongamano ya uwekezaji, akisisitiza kuwa mikutano hiyo inapaswa kuzaa tija, ufanisi na mikataba halisi ya biashara kati ya Serikali na wafanyabiashara wa ndani kupitia Miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).

Amesema zaidi ya theluthi mbili ya mahitaji ya uwekezaji katika Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano, sawa na Sh334 trilioni kati ya Sh477 trilioni, zinatarajiwa kutoka sekta binafsi. Aidha, katika mipango ya awali, Sh21.03 trilioni zilikadiriwa kupatikana kupitia PPP, kutoka katika mchango wa sekta binafsi uliopangwa kufikia Sh40.6 trilioni.

Kisanga amesema TNCC imejipanga kuwa daraja la kuwawezesha wafanyabiashara wa Kitanzania kushiriki kikamilifu katika miradi hiyo badala ya kubaki watazamaji. Amesema programu hiyo iliyoanza Pwani inalenga kufika mikoa yote nchini kwa ajili ya kubaini miradi ya kimkakati, kuandaa muhtasari na maandiko ya biashara, kufanya tafiti za uwezekano wa miradi pamoja na kuendesha kliniki za uwekezaji na majukwaa ya biashara kati ya Serikali na wafanyabiasha.





No comments