SERIKALI YAKIRI WAKULIMA NA WAFUGAJI WAMECHANGIA UHIMILIVU WA UCHUMI NA USALAMA WA CHAKULA



Serikali imeeleza kuwa Wakulima na Wafugaji wamechangia kuleta  uhimilivu wa uchumi na usalama wa chakula kutokana na uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo yanayotosheleza mahitaji ya nchi hatua ambayo imetajwa kulifanya taifa kuwa na utulivu wakati huu ambao kuna vita kubwa za kiuchumi duniani.


Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa  wakati wa kufungua Kongamano la Kitaifa la Wakulima Wadogo na Mkutano Mkuu wa 31 wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima  (MVIWATA) itakayofanyika kwa siku tatu kuanzia Leo 29 Septemba hadi Oktoba Mosi , 2026 Mkoani Morogoro.


Balozi Dkt. Bashiru amesema nchi inajivunia kuwa na wakulima na wafugaji wanaozalisha chakula cha kutosha ambao wamekuwa nguzo muhimu katika kuimarisha usalama wa chakula na kueleza umuhimu wa kujadili changamoto zinazowakabili wakulima wadogo, ikiwemo uhakika wa ardhi, kilimo ikolojia na masoko ya mazao, katika jitihada za kuelekea uhuru wa chakula. 


Aidha, ametumia jukwaa hilo kutoa onyo kwa wakulima na wafugaji kuacha kujichukulia sheria mkononi na kusababisha uhasama unaoweleta madhara baina yao ikiwemo kujeruhiana na vifo huku akiitaka MVIWATA kutafuta taarifa sahihi kuhusu tahadhari na namna ya kukabiliana na Mvua za El Nino, hatua itakayopunguza upotoshaji unaowapa hofu wakulima na wafugaji.


Katika hatua nyingine, ameupongeza MVIWATA kwa kutimiza miaka 33 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 na kuendelea kufanya mikutano yake mikuu kila mwaka tangu kusajiliwa rasmi mwaka 1995.


Baadhi ya Wananchi ambao ni Wanamchama wa MVIWATA wametoa kero zao zinazohitaji utatuzi wa haraka, ambapo Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameahidi kuipeleka serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi.


Mwenyekiti anayemaliza Muda wake wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) Bw. Apollo Chamwela ameomba serikali kwa kushirikiana na wadau kuangalia namna ya kuwakopesha ng'ombe wa maziwa wakulima wadogo ili waweze kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na usalama wa chakula kwa ujumla.


Akijibu  Ombi la Mwenyekiti wa MVIWATA anayemaliza muda wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema serikali kwa kushirikiana na  Benki, Viwanda vya maziwa zinazotekeleza mradi wa Kopa Ng'ombe Lipa Maziwa ili kukaa na kujadili namna ya kupanua wigo wa  ukopeshaji wa ng'ombe wa maziwa ili kuongeza uzalishaji katika mazao kupitia mbolea itakayozalishwa na Ng'ombe.







No comments