SERIKALI YASISITIZA TEKNOLOJIA NA UWEKEZAJI KUONGEZA THAMANI YA MADINI
Serikali imesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kisasa na uwekezaji katika kuongeza tija, usalama na thamani ya madini nchini, huku ikiwasisitiza wadau wa sekta hiyo kuwajibika kwa pamoja kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania na kuchangia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, leo, Septemba 27, 2026, wakati akifungua rasmi Maonesho ya Tisa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Bombambili, Geita.
Dkt. Kiruswa amesema kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu, “Madini ni Utajiri – Tuwajibike kwa Pamoja Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” inaweka wajibu kwa Serikali, wawekezaji, wachimbaji na wananchi kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa tija na manufaa mapana kwa taifa.
Amesisitiza kuwa maonesho hayo yanapaswa kuwa chachu ya kubadilisha fursa na maazimio kuwa miradi, ubia na matokeo yanayopimika, badala ya kubaki katika majadiliano pekee.
“Uwajibikaji unahusisha matumizi ya teknolojia sahihi, uzingatiaji wa sheria, usalama na afya migodini, utunzaji wa mazingira, pamoja na kuhakikisha jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji zinapata manufaa stahiki,” amesema Dkt. Kiruswa.
Akizungumzia utafiti wa madini, Dkt. Kiruswa amesema Serikali inalenga kupanua Utafiti wa Kina wa Jiofizikia kwa Kutumia Ndege (High-Resolution Airborne Geophysical Survey) ili kufikia angalau asilimia 50 ya eneo la nchi ifikapo mwaka 2030, kutoka takribani asilimia 16 ya sasa.
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza uchimbaji wa kubahatisha, gharama za utafutaji wa madini na hatari ya wachimbaji wadogo kupoteza mitaji yao.
Ameongeza kuwa Serikali imetunga sheria inayoelekeza asilimia 10 ya mapato yatokanayo na shughuli za madini kutengwa kwa ajili ya tafiti za jiosayansi.
Dkt. Kiruswa amesema Wizara ya Madini imeandaa Mkakati wa Uongezaji Thamani wa Madini wa 2026/27–2030/31, unaolenga kuimarisha uchakataji, uchenjuaji na usafishaji wa madini nchini kwa kushirikiana na TISEZA, hatua inayolenga kuongeza ajira, uwekezaji na fursa za biashara kwa Watanzania.
Amezisifu kampuni za madini zinazozingatia kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini akisema maboresho ya kanuni hizo yameongeza idadi ya kampuni za Kitanzania zinazotoa bidhaa na huduma katika migodi.
Aidha, Dkt. Kiruswa amewahimiza vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum kutumia fursa zinazotolewa kupitia Programu ya Madini kwa Kesho Njema (Mining for a Brighter Tomorrow – MBT), inayotoa fursa za leseni, ushauri wa kitaalamu, taarifa za utafiti na kwa miradi yenye sifa, vifaa na mitambo.
“Lengo la Serikali ni kuona makundi haya yanakuwa washiriki wa maendeleo ya sekta, na siyo watazamaji wa maendeleo hayo,” amesema.
Dkt. Kiruswa pia amewahimiza wadau wa sekta ya madini kujisajili mapema ili kushiriki katika Mkutano wa 7 wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC 2026), akisema mkutano huo utatoa fursa kwa wawekezaji, wataalamu na wadau mbalimbali kujenga ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kujadili fursa za uwekezaji katika sekta ya madini nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, amesema Geita inaendelea kuwa kitovu cha matumizi ya teknolojia za kisasa katika shughuli za madini nchini, akieleza kuwa maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za kuonesha na kukuza matumizi ya teknolojia, ubunifu na suluhisho za kisasa katika shughuli za uchimbaji na huduma zinazohusiana na madini.
Mnyeti amesema sekta ya madini ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya ajira na maendeleo ya kiuchumi mkoani Geita, hivyo amewahimiza vijana kutumia fursa ya maonesho hayo kujifunza teknolojia, ubunifu na fursa mbalimbali zinazotokana na sekta hiyo ili kujenga uwezo na kushiriki kikamilifu katika shughuli za madini.

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Post a Comment