ZMBF YAENDELEA KUWEKEZA KATIKA KUPAMBANA NA VIFO VYA WAJAWAZITO ZANZIBAR



Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), kwa kushirikiana na WAJAMAMA na washirika mbalimbali, ipo katika maandalizi ya uzinduzi wa kampeni ya “Mwanzo Wake” (Their Beginning), yenye lengo la kuimarisha lishe ya mama wakati wa ujauzito, kuongeza uchunguzi wa mapema na kupunguza changamoto ya upungufu wa damu kwa wanawake wajawazito Zanzibar, ambayo ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuchangia vifo vya wajawazito.



Akizungumza pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 81), jijini New York, Septemba 22, 2026, Mjumbe wa Bodi ya ZMBF, Dkt. Ellen Mkondya-Senkoro, aliyemwakilisha Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa ZMBF, Mama Mariam Mwinyi, amesema kampeni hiyo inalenga kuifanya lishe ya mama kuwa jukumu la familia na jamii, huku ikihamasisha matumizi ya rasilimali za ndani zenye virutubisho, ikiwemo dagaa na mwani.



Aidha, Dkt. Ellen amesema Zanzibar imepiga hatua katika kupunguza vifo vya wajawazito, ambapo kiwango hicho kimeshuka kutoka vifo 307 hadi 119 kwa kila vizazi hai 100,000, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuchukua hatua madhubuti ili kupunguza zaidi vifo hivyo.



Amesema takribani wanawake 60,000 hujifungua Zanzibar kila mwaka, huku karibu wanawake saba kati ya 10 wakikabiliwa na upungufu wa damu wakati wa ujauzito.



Dkt. Ellen amesema ZMBF, kwa kushirikiana na WAJAMAMA, inayoongozwa na Bi. Nafisa Jidawi, inalenga kuanzisha kampeni ya Mwanzo Wake, ambayo itajikita katika kuimarisha lishe ya mama, uelewa wa familia na uchunguzi wa mapema wa changamoto za kiafya wakati wa ujauzito.



Amesema mikakati hiyo inajengwa juu ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuimarisha miundombinu ya afya, upatikanaji wa vifaa tiba na huduma za afya kwa wananchi.



Halikadhalika, amesema mpango huo unaunga mkono juhudi za Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi, katika kuimarisha Maendeleo ya Awali ya Mtoto, pamoja na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha afya ya mama na mtoto barani Afrika.



Vilevile, Dkt. Ellen ametoa wito kwa wafadhili, taasisi na washirika wa maendeleo duniani kuunga mkono suluhisho zinazotokana na jamii na kuongeza uwekezaji katika programu zinazolenga kuimarisha afya na kuokoa maisha ya mama na mtoto.



Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt.Elsie S  Kanza.








No comments