TANZANIA KUFANYA MAPINDUZI YA KIMKAKATI KATIKA SEKTA YA MAFUTA NA GESI

 


Waziri wa Fedha  Balozi Khamis Mussa Omar amesisitiza umuhimu wa Serikali kufanya mapitio ya kimkakati katika matumizi ya rasilimali za mafuta na gesi ili kuleta tija zaidi kwa wananchi na bara la Afrika kwa ujumla.

Balozi Omar amesema hayo wakati akiongoza kikao cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 11 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Uwekezaji wa Miunombinu ya Asia (AIIB), unaofanyika Doha nchini Qatar, kikao kilichofanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini humo.

Amebainisha kuwa wakati umefika kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika zenye rasilimali hizo, kama Msumbiji, kuanza kufikiria namna ya kutumia gesi asilia kuzalisha mbolea kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya ndani badala ya kutegemea zaidi soko la nje.

Amesema kuwa matukio ya kimataifa, ikiwemo changamoto za usafirishaji katika mifereji mikuu ya dunia kama Strait of Hormuz, Suez na Panama, yametoa funzo kwa mataifa ya Afrika kuwa na utegemezi mdogo wa masoko ya kimataifa na badala yake kuimarisha uchumi wa ndani.

Kuhusu ajira, ilibainishwa kuwa ni jambo la faraja kuona Watanzania wengi wakipata ajira za staha nchini humo, huku kukiwa na takwimu zinazoonyesha kuwepo kwa Watanzania zaidi ya 2,500 katika maeneo hayo.

Aidha, amesisitiza haja ya kujifunza zaidi kutoka kwa mataifa ya Mashariki ya Kati kuhusu uchumi wa kemikali za mafuta, akibainisha kuwa ingawa Tanzania ilijifunza mengi kutoka Norway kupitia programu ya Oil for Development, sasa ni wakati wa kupanua wigo wa maarifa ili kuimarisha uchumi wa Taifa.

Ameupongeza Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar kwa kutimiza na kuadhimisha miaka 10 ya uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi na nchi hiyo, hatua ambayo alisema ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na maendeleo ya sekta ya nishati na sekta nyingine .






No comments