TANZANIA YASHIRIKI UFUNGUZI WA MAFUNZO YA SSTC KUHUSU UKUZAJI WA BIASHARA NA UWEKEZAJI KWA NCHI ZA AFRIKA
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Macocha Moshe Tembele, ameshiriki katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo yanayotolewa chini ya Programu ya Ushirikiano wa Kusini-Kusini na wa Pande Tatu (South-South and Triangular Cooperation – SSTC) kuhusu Uhamasishaji wa Biashara na Uwekezaji kwa Nchi za Afrika, yanayofanyika Septemba 28, 2026 katika Kituo cha Maendeleo ya Rasilimali Watu kwa Huduma za Mauzo ya Nje na Biashara, Jakarta.
Programu hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Indonesia kupitia Wizara ya Biashara na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) kwa lengo la kuimarisha uwezo wa nchi za Afrika katika kukuza biashara na uwekezaji, sambamba na kuwezesha ubadilishanaji wa maarifa, uzoefu na mbinu bora katika maendeleo ya biashara.
Mafunzo hayo yanajikita katika maeneo mbalimbali, yakiwemo uwezeshaji wa biashara, maendeleo ya mauzo ya nje, majadiliano ya kibiashara, uhamasishaji wa uwekezaji, ushiriki wa biashara ndogo na za kati, pamoja na ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda.
Aidha, washiriki watapata fursa ya kujifunza kwa vitendo kupitia majadiliano na wataalamu, viongozi wa Serikali na wawakilishi wa sekta binafsi, pamoja na kufanya ziara katika taasisi na kampuni mbalimbali nchini Indonesia.
Programu hiyo inashirikisha washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika, zikiwemo Tanzania, Ethiopia, Rwanda, Msumbiji na Somalia.
Hafla ya ufunguzi imehudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo Mabalozi wa nchi za Afrika, maafisa wa Serikali ya Indonesia, wawakilishi wa JICA, pamoja na wadau wengine kutoka sekta za biashara na uwekezaji.
Kupitia programu hiyo, nchi washiriki zinatarajiwa kuimarisha ushirikiano, kujenga uhusiano endelevu wa kitaasisi, pamoja na kubadilishana maarifa na uzoefu katika kukuza biashara na uwekezaji.

Post a Comment