TANZANIA YATOA WITO KWA DUNIA KUFANYA KWA VITENDO AHADI YA KUKABILI ATHARI ZA KUPANDA KWA KINA CHA BAHARI
Tanzania imetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuongeza kasi ya upatikanaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi, teknolojia na mifumo madhubuti ya tahadhari za mapema ili kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na athari zinazoongezeka za kupanda kwa kina cha bahari.
Akihutubia Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kupanda kwa kina cha Bahari mjini New York, Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi, amesema tatizo hilo si tishio la siku zijazo tena, bali tayari linaathiri maisha ya watu, uchumi na mifumo ya ikolojia duniani.
Kwa Tanzania, athari hizo ni kubwa kutokana na ukanda wake wa pwani ya Bahari ya Hindi, Zanzibar na visiwa vingine ambavyo vinategemewa na mamilioni ya watu kupitia uvuvi, utalii na biashara. Mmomonyoko wa fukwe, kuingia kwa maji ya chumvi katika vyanzo vya maji baridi na mafuriko vinatajwa kuwa miongoni mwa vitisho kwa wananchi, miundombinu na mafanikio ya maendeleo ya nchi.
Makamu wa Rais ameeleza kuwa, Tanzania tayari inachukua hatua kwa kuimarisha ulinzi wa pwani, kurejesha mikoko na mifumo ya ikolojia, kuimarisha usalama wa maji na kuendeleza mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi inayoongozwa na jamii.
Hata hivyo, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa juhudi za nchi moja moja hazitoshi, akitaka fedha za tabianchi kuwa za kutosha, za uhakika na zinazopatikana kwa urahisi zaidi kwa nchi zinazoendelea na jamii za pwani zilizo katika mazingira hatarishi.
Mkutano huo wa Septemba 24, 2026, umezikutanisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, Viongozi, Wataalamu na Wadau wengine kuweka msimamo wa pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa dhidi ya tishio la kupanda kwa kina cha bahari. Mkutano huo unafanyika ikiwa ni mwendelezo wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa mwaka 2024 uliolifanya suala hilo kuwa ajenda muhimu ya kimataifa.
Makamu wa Rais yuko New York nchini Marekani, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.



Post a Comment