TIA YAWAANDAA WANAFUNZI KWA AJIRA NA UJASIRIAMALI.



TAASISI ya Uhasibu Tanzania (TIA),imeendelea kuwaandaa wanafunzi wake kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na ujasiriamali kupitia programu ya Ukuzaji na Uendelezaji wa Wanafunzi Kitaaluma na Kitaalamu, inayolenga kuwajengea uwezo zaidi ya kupata vyeti vya kitaaluma.


Kupitia programu hiyo, zaidi ya wanafunzi 5,000 wamefikiwa kwa kushiriki warsha zinazohusu ujasiriamali, ubunifu, ajira pamoja na fursa za kimataifa.


Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. William Amos Pallangyo,amesema hayo Septemba 7,2026, Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 na mwelekeo wa 2026/2027.


Amesema  zaidi ya wanafunzi 500 wamepatiwa mafunzo mahsusi ya ujasiriamali, huku takribani 100 kati yao wakisaidiwa kuanzisha biashara ndogo ndogo.


Aidha amesema Taasisi hiyo pia imeendelea kuwajengea wanafunzi uwezo wa kutumia mifumo inayotumika katika mazingira halisi ya kazi, ikiwemo Tally ERP, NeST System na QuickBooks, hatua inayolenga kuwafanya wahitimu kuwa na ujuzi unaoweza kutumika moja kwa moja wanapoingia kwenye soko la ajira.


TIA imesema mpango huo unaendana na mabadiliko ya mtazamo wa elimu kutoka kujikita katika kupata cheti pekee, kwenda katika kutoa maarifa na ujuzi unaoweza kutumika katika ajira, biashara na kutatua changamoto mbalimbali za jamii.




No comments