Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), wapewa nafasi ya kuendeleza ubunifu wa teknolojia ya kuzalisha gesi ya haidrojeni
Mbunifu Lusano Luvanda, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), amepewa nafasi ya kuendeleza ubunifu wa teknolojia ya kuzalisha gesi ya haidrojeni kwa kutumia maji na malighafi zinazopatikana nchini, baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, kuitaka menejimenti ya chuo hicho kufanya tathmini ya kina ya teknolojia hiyo ndani ya mwezi mmoja.
Profesa Mkenda ametoa agizo hilo Oktoba 9, 2026, wakati wa ziara yake MUST mkoani Mbeya, ambapo ametembelea bunifu mbalimbali zinazofanywa na wanafunzi na watafiti, ikiwemo teknolojia ya kuzalisha gesi inayobuniwa na Luvanda.
Amesema tathmini hiyo inapaswa kufanywa na jopo la wanasayansi kutoka MUST kwa kushirikiana na taasisi nyingine za elimu na utafiti, ili kubaini usalama wa teknolojia hiyo, ufanisi wake na uwezekano wa kuitumia katika shughuli za kupikia na huduma nyingine.
Profesa Mkenda amesisitiza kuwa ni muhimu kulinda haki miliki ya Luvanda wakati tathmini na hatua za kuendeleza teknolojia hiyo zikiendelea, akieleza kuwa ubunifu wa Watanzania unapaswa kupewa nafasi ya kukua na kufikia hatua ya kuzalisha bidhaa zinazoweza kutumika kibiashara.
Vilevile, ameitaka menejimenti ya MUST kuhakikisha hatua za kusajili kampuni ya Eco Flame Clean Energy, inayohusishwa na ubunifu huo, zinafanyika mapema ili, endapo tathmini ya kisayansi itathibitisha usalama na ufanisi wa teknolojia hiyo, kampuni iweze kuanza uzalishaji na usambazaji wa gesi kwa taasisi zinazohitaji.
Luvanda, ambaye ni mmoja wa wabunifu walioibuka kupitia MUST, alihitimu kidato cha nne mwaka 2021 katika Shule ya Sekondari ya Serikali Forest mkoani Mbeya, kabla ya kujiunga na MUST mwaka 2022 kusomea kozi ya Kilimo Biashara na Teknolojia, na kuhitimu ngazi ya diploma mwaka 2025.




Post a Comment