Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) latwaa tuzo nne za umahiri katika mawasiliano kwa umma
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanikiwa kutwaa tuzo nne za umahiri katika mawasiliano kwa umma, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuboresha eneo la utoaji wa taarifa, kuimarisha mawasiliano ya kimkakati na kutumia ubunifu katika kuwafikishia wananchi taarifa kwa ufanisi.
Akizungumza Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange mara baada ya kupokea tuzo hizo katika Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST), Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowelle, amesema mafanikio hayo ni heshima kubwa kwa Shirika na chachu ya kuendelea kubuni njia bora za mawasiliano pamoja na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema TANESCO itaendelea kutumia teknolojia na majukwaa ya kidijitali kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, kwa wakati na kwa njia rahisi, za kisasa na zenye ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Savera Kazaura, aliyemwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, ameipongeza TANESCO kwa mafanikio hayo na kwa hatua kubwa iliyopiga katika kuboresha utoaji wa taarifa kwa wananchi, hususan wakati wa changamoto za huduma ya umeme.
Amesema taasisi za umma zinapaswa kuendelea kuwekeza katika mawasiliano ili kuongeza uelewa kwa wananchi na kuimarisha uhusiano kati ya serikali na jamii.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

Post a Comment