MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ameliomba Bunge kuangalia upya sheria na taratibu za manunuzi



MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ameliomba Bunge kuangalia upya sheria na taratibu za manunuzi ili kurahisisha upatikanaji wa fedha na vifaa vya miradi ya maendeleo, akisema ucheleweshaji wake unasababisha miradi kutokamilika kwa wakati.


Nyongo amesema hayo baada ya kukagua ujenzi wa Chuo cha VETA kinachojengwa Kata ya Kazimzumbwi, wilayani Kisarawe, ambapo amesema moja ya changamoto ni kuchelewa kwa fedha na taratibu za manunuzi, hali inayosababisha ujenzi kusuasua tangu 2023.  


Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Saidi Masoud Kisiki, amesema ujenzi unatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa majengo tisa. 


Amesema ujenzi umefikia asilimia 68.3, huku majengo manane yakiwa yamesimama kusubiri vifaa ambavyo mchakato wa manunuzi yake unaendelea katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.


Kisiki amesema mradi huo pia unakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji, barabara na umeme, huku Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, akisema tayari wamewasiliana na TARURA kuhusu barabara kuelekea chuoni hapo na hatua za kuishughulikia zinaendelea.


Naye Mbunge wa Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, amesema kukamilika kwa chuo hicho kutatoa fursa kwa vijana kupata elimu ya ufundi na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri, kuajiriwa au kuajiri wengine, sambamba na kukidhi mahitaji ya viwanda vinavyoendelea kuanzishwa wilayani humo.






No comments