Waziri Dkt.Homera, azindua mifumo mipya ya kuhudumia wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)


 

Waziri wa Nishati,Dkt. Juma Homera, amezindua mifumo mipya ya kuhudumia wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),pamoja na Mkataba wa Huduma kwa Wateja ulioboreshwa, ikiwa ni hatua inayolenga kuhakikisha wateja wakubwa na wadogo wa Shirika hilo wanapata huduma kwa haraka na urahisi.


Akizindua mifumo hiyo jijini Dar es Salaam Oktoba 6, 2026, Dkt. Homera amesema TANESCO imeonesha dhamira ya kupiga hatua zaidi katika kuboresha huduma kwa wateja, akieleza kuwa hatua hiyo ina umuhimu mkubwa katika maslahi ya Taifa, hususan katika utekelezaji wa Dira 2050 na maono ya Rais,Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha taasisi zinatumia ubunifu na teknolojia katika kuboresha huduma kwa wananchi.


Mifumo aliyoizindua ni pamoja na 'Twiga Assistant' suluhisho la kisasa linalotumia akili mnemba (AI) na kumwezesha mteja kupata huduma saa 24 kwa siku bila kulazimika kupiga simu TANESCO na  'Twiga Premium Portal' jukwaa maalum la kidijitali litakalowawezesha wateja wakubwa kupata huduma mbalimbali kwa urahisi zaidi.


Aidha, Dkt. Homera amezindua namba maalum 185 kwa ajili ya wateja wakubwa, itakayowawezesha kupata huduma za haraka, za moja kwa moja na zenye kipaumbele pamoja na uzinduzi wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja Wakubwa ili kuhakikisha kundi hilo linapata huduma zinazokidhi mahitaji yake.


Pamoja na kuipongeza TANESCO kwa ubunifu huo uliofanywa na wataalamu wa ndani, Dkt. Homera amelitaka Shirika hilo kuhakikisha Mkataba wa Huduma kwa Wateja unatekelezwa kwa vitendo katika ngazi zote na ahadi zilizomo ndani yake zinakuwa sehemu ya utamaduni wa kazi wa kila mtumishi.


Katika hatua nyingine, Dkt. Homera amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika Sekta ya Nishati umeendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, ambapo uwezo wa kuzalisha umeme umefikia MW 4,606, sawa na ongezeko la asilimia 21.32, huku mahitaji ya juu ya umeme yakifikia MW 2,316, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.97 ikilinganishwa na mwaka 2025.



Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, amesema huduma zilizozinduliwa, zikiwemo Twiga AI Chatbot, Twiga Premium Customer Portal, Premium Customers Toll Free Line, Premium Customer Service Section  pamoja na Mkataba wa Huduma kwa Wateja ulioboreshwa, zinaendana na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa pamoja na kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini, huduma zinazotolewa kwa wananchi zinaendelea kuboreshwa kupitia teknolojia, ubunifu na mifumo ya kisasa.











No comments