OTR YAFUNGUA MILANGO KWA RMB KUSHIRIKI MAGEUZI YA TAASISI ZA UMMA
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) imefungua milango kwa Benki ya Rand Merchant (RMB) kubaini fursa za ufadhili na uwekezaji katika taasisi za umma zilizo chini ya usimamizi wake, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya miradi ya kimkakati na kuimarisha uwezo wa kifedha wa kampuni hizo. Mwaliko huo umetolewa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alipokutana na ujumbe wa benki hiyo ulioongozwa na Mkuu wa Huduma za Kibenki kwa Wateja wa Taasisi katika Ukanda wa Afrika Mashariki, John Njuguna, jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yalijikita katika fursa za ufadhili na uwekezaji kwenye sekta za miundombinu, nishati jadidifu, kilimo, usafirishaji, mawasiliano, madini na dawa, huku yakilenga kutumia utaalamu wa kifedha wa RMB kusaidia taasisi za umma kupata mitaji ya kutekeleza miradi na kupanua shughuli zao. Mchechu amesema OTR iko tayari kuratibu ushirikiano huo kwa kubaini miradi yenye tija kibiashara na kuandaa mifumo ya ufadhili inayokidhi mahitaji ya kila taasisi.
Ameeleza kuwa OTR inasimamia taasisi na kampuni za umma 308, zikiwemo kampuni 252 ambazo Serikali inamiliki hisa nyingi na 56 ambazo inamiliki hisa chache, zenye jumla ya thamani ya uwekezaji wa Sh trilioni 92.3. Amesema Serikali inazihimiza taasisi hizo kuimarisha uwezo wa kujiendesha kifedha kwa kutumia rasilimali walizonazo na kutafuta vyanzo mbadala vya mitaji, ikiwemo mikopo ya benki, hati fungani na uuzaji wa hisa kupitia soko la mitaji.
Kwa upande wake, Njuguna amesema RMB ina nia ya kuimarisha ushirikiano na taasisi za umma nchini, ikitumia uzoefu wake katika kufadhili miradi ya miundombinu na shughuli za kibiashara katika masoko mbalimbali ya Afrika. Amesema vipaumbele vya Tanzania katika maendeleo ya miundombinu na nafasi yake ya kimkakati katika biashara na usafirishaji wa kikanda vinatoa fursa kwa benki hiyo kuchangia kupitia suluhisho za kifedha na uwekezaji.
Naye Mkuu wa Suluhisho za Uwekezaji katika Sekta ya Miundombinu wa RMB kwa Afrika, Sindisiwe Mosoeu, amesema benki hiyo ina mifumo mbalimbali ya ufadhili inayoweza kutumika katika miradi ya taasisi za umma, ikiwemo ufadhili wa miradi, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi pamoja na miradi ya nishati jadidifu. Ameongeza kuwa RMB ina uzoefu wa kufadhili miradi ya nishati ya jua, upepo na maji, huku Mtaalamu wa Uandaaji wa Miundo ya Uwekezaji katika Masoko ya Kimataifa wa benki hiyo kwa Afrika, Sinethemba Mvandamba, akieleza kuwa benki hiyo inaweza kuziunganisha taasisi za umma na vyanzo vya mitaji katika masoko ya kimataifa.

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
Post a Comment