PROF.SHEMDOE AZITAKA HALMASHAURI KUONGEZA UWEKEZAJI KWENYE LISHE.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amezitaka halmashauri nchini kuongeza juhudi katika utekelezaji wa afua za lishe kwa kuimarisha ushirikiano wa sekta mbalimbali na kuhakikisha rasilimali fedha zinazotengwa zinatumika ipasavyo kukabiliana na changamoto za lishe nchini.
Akizungumza katika Mkutano wa 10 wa Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka wa fedha 2025/2026 jijini Dodoma, Prof. Shemdoe amesema ili kufanikiwa katika ajenda hiyo inahitaji viongozi wa mikoa na halmashauri kuendelea kusimamia upatikanaji wa fedha na kuhakikisha zinatumika kutekeleza mipango iliyowekwa, huku akizitaka halmashauri ambazo hazijafanya vizuri kuongeza juhudi na zile zilizopiga hatua kuendelea kuboresha utendaji.
Amesisitiza kuwa lishe si jukumu la sekta ya afya pekee, bali linahitaji ushirikiano wa sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, elimu, maji, hifadhi ya jamii na usafi wa mazingira, kwa kuwa kila moja ina mchango katika kuhakikisha wananchi wanapata lishe bora.
Amesema tathmini hiyo imeonesha mafanikio katika maeneo mbalimbali, yakiwemo kuanza kwa tafiti za kiutendaji kuhusu lishe katika mikoa ya Mtwara, Njombe na Iringa, pamoja na baadhi ya halmashauri kutumia mapato ya ndani kugharamia tafiti hizo.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa vyakula vilivyoongezwa virutubisho, hususan katika shule, huku akizihimiza halmashauri ambazo bado hazijafanya tafiti za lishe kutenga fedha ili kupata takwimu zitakazosaidia kupanga afua kulingana na mahitaji ya wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, Florent Kyombo, amezitaka halmashauri kuongeza bajeti ya lishe katika maandalizi ya bajeti ya mwaka 2027, akisisitiza kuwa kiwango cha chini cha Sh1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano hakipaswi kuwa kikomo cha fedha zinazotengwa.
Kyombo amesema halmashauri zinapaswa kutumia mapato ya ndani kufanya tathmini ya mahitaji yao na kutenga fedha zaidi kulingana na uwezo na vipaumbele vya maeneo husika ili kuboresha huduma za lishe na kupunguza changamoto za utapiamlo.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Post a Comment