Senegal yarejeshewa rasmi ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025



TIMU ya taifa ya Senegal imerejeshewa rasmi ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada ya Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kutoa uamuzi wa kuitambua tena kuwa bingwa wa mashindano hayo.


Uamuzi huo umebatilisha hukumu ya awali iliyokuwa imeivua Senegal ubingwa wa michuano hiyo, ambao iliutwaa uwanjani baada ya kuifunga Morocco, wenyeji wa mashindano hayo, katika fainali iliyokuwa na vurugu na mvutano mkubwa mwezi Januari.


Katika mchezo huo uliofanyika Rabat, Senegal iliibuka na ushindi wa bao 1-0 baada ya dakika 120 za mchezo, ikiwemo muda wa nyongeza.


Hata hivyo, takribani miezi miwili baadaye, matokeo hayo yalibatilishwa na kamati ya rufaa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), iliyoiadhibu Senegal kwa madai ya kukiuka kanuni za mashindano baada ya wachezaji wake kuondoka uwanjani katika dakika za nyongeza za kipindi cha pili, wakipinga uamuzi wa mwamuzi wa kutoa penalti dhidi yao.


Baada ya uamuzi huo, Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) lilikata rufaa CAS, chombo cha juu zaidi cha kisheria katika masuala ya michezo duniani.


Shauri hilo lilisikilizwa na jopo la majaji watatu katika kikao kilichofanyika faraghani mjini Lausanne, Uswisi, Oktoba 8, huku uamuzi wa CAS sasa ukiirejeshea Senegal hadhi yake ya kuwa mabingwa wa AFCON 2025.

No comments