Tanzania kukabidhi ofisi kamati ya CAF ya maandalizi ya Afcon 2027
Tanzania
kesho, Novemba 25, 2026, inatarajiwa kupiga hatua nyingine muhimu katika
maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, baada ya
Ofisi za Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kukabidhiwa
rasmi kwa matumizi ya Kamati Kuu ya Maandalizi ya mashindano hayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, hafla hiyo itafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam,
kuanzia saa 3:00 asubuhi.
Katika hafla hiyo, pia kutashuhudiwa utiaji saini wa Mkataba wa Maelewano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Hatua hiyo inalenga kuweka msingi wa ushirikiano katika maandalizi ya pamoja ya AFCON 2027, ambayo yatahusisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Maandalizi hayo yanatajwa kuwa sehemu muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuonesha uwezo wa nchi za Afrika Mashariki katika kuandaa mashindano makubwa ya soka barani Afrika na duniani.
Wizara hiyo imewahimiza wananchi kufuatilia taarifa za tukio hilo kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kupata maendeleo ya maandalizi ya michuano hiyo mikubwa.
AFCON 2027 inatarajiwa kuwa fursa muhimu kwa Tanzania na nchi washirika katika kukuza michezo, utalii na kuitangaza Afrika Mashariki kimataifa.
Post a Comment