TASAC YASHIRIKI MAADHIMISHO YA WIKI YA USAFIRI ENDELEVU ARDHINI 2026
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo Novemba 24, 2026, limeungana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini, yaliyofanyika katika viwanja vya Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Hafla ya ufunguzi wa maadhimisho hayo, yanayojulikana pia kama Wiki ya LATRA, imeongozwa na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa. Maadhimisho hayo yamewakutanisha taasisi za uchukuzi na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji kwa lengo la kutoa elimu kwa umma na kuimarisha ushirikiano katika mnyororo wa usafirishaji nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Mbarawa ameipongeza LATRA kwa juhudi zilizofanyika katika kuandaa maadhimisho hayo na kuhakikisha yanafanikiwa. Aidha, amezipongeza taasisi, mashirika na kampuni zilizoshiriki kwa kuonesha ubunifu, ushirikiano na dhamira ya pamoja katika kuendeleza sekta ya usafiri nchini.
Amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, kujenga mahusiano ya kibiashara na kubadilishana maarifa yatakayochangia kuboresha huduma za usafiri nchini.
"Maadhimisho haya yanatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, pamoja na kutoa fursa za kujenga mahusiano ya kibiashara na kubadilishana maarifa yatakayosaidia kuboresha huduma za usafiri ardhini. Juhudi hizi zinaendana na mwelekeo wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 katika kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi," amesema Prof. Mbarawa.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Kuharakisha Usafiri Endelevu: Usafiri Salama, Rafiki kwa Mazingira na Jumuishi kwa Wote” (Accelerating Sustainable Transport: Safe, Green and Inclusive Mobility).
Kaulimbiu hiyo inasisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usafiri inayozingatia usalama wa watumiaji, uhifadhi wa mazingira na upatikanaji wa huduma kwa makundi yote ya jamii.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhitimishwa Novemba 26, 2026, yakilenga kuhamasisha matumizi ya mifumo endelevu ya usafiri na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wadau wa sekta ya uchukuzi nchini.
.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)

Post a Comment