WATUMISHI WAASWA KUJENGA TASAC IMARA KUPITIA WELEDI NA UWAJIBIKAJI


 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, amewataka watumishi wa Shirika hilo kuendeleza utamaduni wa weledi, ubunifu na uwajibikaji ili kujenga taasisi imara inayotoa huduma bora katika sekta ya usafiri majini.


Akizungumza leo, Novemba 24, 2026, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha watumishi wa Kurugenzi ya Usalama, Ulinzi wa Vyombo vya Usafiri na Utunzaji wa Mazingira Majini cha TASAC, kinachofanyika Kibaha, mkoani Pwani, amesema Shirika lina jukumu la kuhakikisha usalama, ulinzi na uhifadhi wa mazingira kwa kuzingatia sheria za kitaifa na mikataba ya kimataifa.


Ameeleza kuwa majukumu ya TASAC yanajumuisha kusimamia usalama wa bandari na meli, kudhibiti uchafuzi wa mazingira ya bahari na maziwa, kufuatilia mienendo ya meli za Tanzania katika maji ya kimataifa, pamoja na kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji majini.


Amesisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu hayo unahitaji wataalamu wenye ujuzi na weledi katika masuala ya ubaharia, ukaguzi wa meli, usalama, ulinzi wa vyombo vya usafiri na uhifadhi wa mazingira majini.


"Nguvu ya TASAC ipo kwa watu wake. Tunapojifunza, kushirikishana uzoefu na kuendeleza taaluma zetu kila siku, tunaijenga TASAC imara zaidi yenye uwezo wa kutoa huduma bora kwa wananchi na sekta ya usafiri majini kwa ujumla," amesema Bw. Salum.


Aidha, amewapongeza watumishi wa Kurugenzi hiyo kwa mchango wao katika kutekeleza mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na Serikali, na kuwataka kuendeleza tafiti, ubunifu na kujifunza kutoka kwa wataalamu wenye uzoefu ili kukabiliana na changamoto za sekta.


"Tunahitaji kuwa taasisi inayojifunza kila wakati, inayobuni suluhisho na inayoendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sekta. Mafanikio ya TASAC yatatokana na ubunifu, weledi na uwajibikaji wa kila mtumishi," amesisitiza.


Vilevile, amesema TASAC imejipanga kufanya mageuzi yatakayowezesha kupanua wigo wa huduma zake na kuimarisha nafasi yake kama mamlaka ya usafiri majini nchini.


Ameongeza kuwa dhamira ya Shirika ni kuhakikisha huduma za usafiri majini zinakuwa salama, zenye ufanisi na endelevu, huku zikichochea maendeleo ya uchumi wa buluu na Taifa kwa ujumla.

No comments