KAMATI YA BUNGE YAPITISHA RANDAMA YA MADINI MWAKA 2026/2027
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imepitisha Randama ya Wizara ya Madini kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka wa fedha 2026/2027,na kuipongeza Wizara hiyo kwa namna inavyosimamia utekelezaji wa majukumu yake yaliyopelekea kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa kufikia asilimia 12.7 katika robo ya tatu ya Julai hadi Septemba 2025.
Pia imepongezwa kwa namna inavyodhibiti utoroshaji wa madini na biashara haramu ya madini nchini, hatua ambayo imepelekea kukamatwa kwa madini ya aina mbalimbali yenye thamani ya shilingi trilioni 2.190.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Subira Mgalu,ametoa pongezi hizo katika kikao kilichofanyika Machi 26,2026,Jijini Dodoma, ambacho pia kimepokea taarifa ya utekelezaji wa Wizara kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026 kwa mwaka 2025/2026.
"Kamati inawapongeza sana Wizara kwa namna mnavyosimamia utekelezaji wa majukumu yenu,mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka,na matokeo ya mchango wa Sekta hii kwenye maendeleo na uchumi wa nchi yanaonekana dhahiri,"amesema.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025/2026, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Madini, Augustino Olal, ameieleza kamati kuwa thamani ya mauzo ya madini na bidhaa za madini nje ya nchi mwaka 2024 ilikuwa dola za Marekani milioni 4,119.9 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 3,551.4 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 16.0.
Pia ameieleza kamati hiyo kuwa makusanyo ya maduhuli yaliyokusanywa na kuwasilishwa Hazina kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026 yameongezeka hadi kufikia shilingi 880,711,819,180.04 ikilinganishwa na shilingi 690,757,642,936.80 katika kipindi kama hicho mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 27.50.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali katika kikao hicho, ameihakikishia kamati kuhusu kutekelezwa kwa mipango yote iliyopangwa na Wizara, ikiwemo ununuzi wa helikopta kwa ajili ya shughuli za utafiti, na kuishukuru kwa namna inavyoisimamia Wizara na kusema mafanikio hayo yametokana na maelekezo na usimamizi mzuri wa kamati hiyo.
Post a Comment