WANAWAKE TASAC WATEMBELEA WODI YA WATOTO NJITI

Wanawake wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) wametembelea Kitengo cha Watoto Njiti (Kangaroo Project) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukabidhi mahitaji mbalimbali kwa watoto wanaohudumiwa katika wodi hiyo.

Ziara hiyo ni sehemu ya kuendeleza maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika tarehe 8 Machi 2026.
Wanawake wa Shirika wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Shirika, Bi. Pili Mazoea, wametekeleza shughuli ya kijamii kwa kutoa msaada katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani 2026. 

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Bi. Mazoea alisema Shirika linaendelea kudumisha utamaduni wa kushirikiana na jamii kwa kutoa huduma na misaada mbalimbali, hususan katika kipindi hiki cha maadhimisho chenye kaulimbiu “Haki na Ustawi kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050.” 

Alieleza kuwa lengo ni kuboresha ustawi wa familia na kuchangia jitihada za Serikali katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususani katika kukuza uchumi wa bluu.

Aidha, alitoa shukrani kwa Bodi ya Wakurugenzi, Mkurugenzi Mkuu pamoja na Menejimenti ya Shirika kwa kuendelea kuwa chachu kwa wanawake wa TASAC kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na ujenzi wa Taifa lenye afya bora.

Katika tukio hilo, wanawake hao walikabidhi vifaa vya matibabu pamoja na mahitaji mengine muhimu, na kuahidi kuendeleza ushirikiano na taasisi husika kwa manufaa ya jamii.

Kwa upande wake Msimamzi wa Kitengo hicho, Bi. Selina Lipipa ameishukuru TASAC kwa kujitoa kwao na kuona  umuhimu wa kushiriki katika utoaji wa huduma kwa  jamii na Serikali kwa ujumla kwani vifaa tiba ambavyo wamepatiwa vitaenda kuongeza wigo wa huduma bora, ufanisi katika kazi  na kuokoa maisha ya watoto hao.

No comments