MAPIGANO MAKALI YAZUKA KATI YA AFGHANISTAN NA PAKISTAN
Mapigano makali yameendelea kati ya vikosi vya Afghanistan na Pakistan katika maeneo ya mpakani, huku mashambulizi ya Anga yakiripotiwa kulenga kambi ya zamani ya jeshi la Marekani ya Bagram, Kaskazini mwa Kabul.
Kwa mujibu wa maafisa wa Afghanistan, mapigano hayo yameongezeka tangu wiki iliyopita baada ya Afghanistan kuanzisha operesheni mpakani, hatua iliyojibiwa na Pakistan kwa mashambulizi ya ardhini na angani.
Idara ya habari ya mkoa wa Nangarhar imesema raia wawili wameuawa katika mashambulizi ya droni, huku wakazi wakiripoti milipuko na milio ya risasi usiku kucha katika maeneo kadhaa.
Msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid, amesema mifumo ya kupambana na ndege imelenga ndege za Pakistan angani.
Wakati huo huo, Naibu Msemaji wa serikali, Hamdullah Fitrat, amedai kuwa mashambulizi ya Pakistan yamesababisha vifo vya raia 36 tangu Alhamisi, madai ambayo Islamabad haijayajibu.
Hali ya taharuki inaendelea katika mpaka huo muhimu wa Torkham huku ulinzi ukiimarishwa mjini Kabul.

Post a Comment