TAKUKURU NA TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA ZASAINI MKATABA KUDHIBITI RUSHWA

TAASISI  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, zimesaini makubaliano ya ushirikiano yatakayolenga kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa katika vyama vya ushirika nchini. 

Hatua hiyo inalenga kuimarisha uwajibikaji, uwazi na kurejesha imani ya wanachama wa ushirika.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo Jijini Dodoma, Msajili na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, amesema sekta ya ushirika imekuwa ikikabiliwa na changamoto za usimamizi wa rasilimali, ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangiwa na vitendo vya rushwa.

Amesema wanachama wengi wamekuwa wakiweka fedha, mazao na rasilimali zao katika vyama vya ushirika kwa matarajio ya kunufaika, lakini vitendo vya rushwa vimekuwa vikikwamisha malengo hayo na kupunguza imani yao.

“Ushirikiano huu unalenga kukomesha vitendo vya rushwa na kurejesha matumaini ya wanachama tumejipanga kuhakikisha tunazuia vitendo hivi kabla havijatokea badala ya kusubiri hadi madhara yatokee,” alisema Dkt. Ndiege.

Aidha, amesisitiza kuwa juhudi hizo zitahusisha utoaji wa mafunzo kwa viongozi na wanachama wa vyama vya ushirika ili kuongeza uelewa wa sheria, kanuni na taratibu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, amesema rushwa ni adui wa maendeleo na utawala bora, hivyo makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo hivyo katika sekta ya ushirika.

Amebainisha kuwa kupitia ushirikiano huo, taasisi hizo mbili zitatekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu ya kupinga rushwa, kufanya tafiti na uchambuzi wa mifumo ya utendaji wa vyama vya ushirika ili kubaini mianya ya rushwa, pamoja na kuandaa vikao kazi vya mara kwa mara kujadili na kufuatilia utekelezaji wa mikakati hiyo.

Hatua hiyo inatarajiwa kuleta mageuzi chanya katika vyama vya ushirika kwa kuimarisha uadilifu, kulinda rasilimali za wanachama na kuongeza imani ya wananchi katika mfumo wa ushirika nchini.

No comments