DODOMA KUANZA AWAMU YA PILI YA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA

 


‎Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, ametangaza kuanza kwa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma kupitia Kampeni ya ‘Msaada wa Kisheria ya Mama Samia’ awamu ya Pili kuanzia Mei Mosi hadi 15,2026.


‎Utekelezaji wa Kampeni hiyo ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais.Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha upatikanaji wa haki kupitia huduma za msaada wa kisheria kwa makundi yenye uhitaji zaidi hususan wanawake, watoto, wazee, watu wenye ulemavu na vijana.


Akizungumza na waandishi wa habari April 30,2026,Senyamule amesema katika utekelezaji uliofanyika 2023, Mkoa ulipata bahati ya kuwa wa kwanza kuanza utekelezaji wa Kampeni hiyo yenye manufaa makubwa kwa wananchi.


Amesema kupitia utekelezaji huo jumla ya wananchi 86,947 wakijumuisha Wanaume 42,298 na Wanawake 44,649 walifikiwa na kupatiwa huduma za Msaada wa Kisheria.


‎Aidha, kati ya migogoro 818 iliyopokelewa, migogoro 452 ilitatuliwa na migogoro 366 inaendelea kufanyiwa kazi.


Pamoja na mafanikio hayo, Serikali imeona bado kuna uhitaji na umuhimu wa kuendeleza juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za msaada wa kisheria kwa urahisi na kwa wakati.


‎Amesema huduma zitatolewa bila malipo ikiwemo  ushauri wa kisheria, elimu ya masuala ya kisheria, uandaaji wa nyaraka za kisheria, uwakilishi Mahakamani na katika Mabaraza kwa wananchi wenye mashauri au wanaotaka kufungua mashauri, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala na huduma ya usajili wa vyeti vya kuzaliwa na vifo kupitia RITA.


‎Kauli Mbiu ya Kampeni hiyo ni, “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo” ambayo ina akisi maono ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka, 2050 inayolenga kujenga jamii yenye usawa, haki na ustawi wa wote.

No comments