HUDUMA ZA DIALYSIS NJOMBE KUPUNGUZA ADHA YA WAGONJWA WA FIGO KUSAFIRI MIKOA YA MBALI



Wananchi wa Mkoa wa Njombe wanaohitaji huduma za usafishaji wa damu kwa wagonjwa wa figo (dialysis) sasa watanufaika na huduma hiyo ndani ya mkoa wao baada ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe kuanza rasmi kuitoa, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama, muda wa safari na usumbufu wa kufuata matibabu katika mikoa mingine.

Akizungumza Julai 7, 2026 wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya sekta ya afya na utoaji wa huduma kwa wananchi, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, alisema Serikali inaendelea kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi ili kuongeza upatikanaji wa matibabu bora nchini.

Dkt. Samizi alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika kuimarisha hospitali za rufaa za mikoa, ikiwemo kuhakikisha huduma za dialysis zinapatikana katika kila hospitali ya rufaa ya mkoa.

Alisisitiza kuwa hospitali ambazo bado hazijaanza kutoa huduma hiyo zinapaswa kuharakisha maandalizi ya miundombinu, vifaa tiba na wataalamu ili wananchi kote nchini waweze kupata huduma hizo bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe alisema hospitali tayari imeweka mashine 12 za dialysis na imeanza kutoa huduma kwa wagonjwa, hatua ambayo itasaidia kupunguza msongamano katika hospitali nyingine pamoja na kuboresha huduma kwa wagonjwa wa figo.













No comments