HUDUMA BURE ZA AFYA NA SHERIA ZAVUTIA MAELFU SABASABA 2026



Maelfu ya wananchi wanaotembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026) wameendelea kunufaika na huduma mbalimbali za afya na ushauri wa kisheria zinazotolewa bila malipo na taasisi za Serikali pamoja na wadau wengine, huku huduma hizo zikionekana kuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vya maonesho ya mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, alipotembelea maonesho hayo amesema wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kupata huduma muhimu zinazopatikana katika eneo moja, ikiwemo uchunguzi na matibabu ya macho bila malipo, pamoja na ushauri wa kisheria hususan katika masuala ya ardhi na changamoto nyingine zinazowakabili.

Amesema maonesho ya mwaka huu, yanayoadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, yamewakutanisha washiriki kutoka zaidi ya mataifa 25 na kutoa fursa kwa wananchi kujifunza teknolojia mpya, kupata huduma za Serikali na sekta binafsi pamoja na kununua bidhaa kwa bei za maonesho.

Kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi, Chalamila amesema Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam inatafakari uwezekano wa kuongeza muda wa maonesho hayo ili watu wengi zaidi wapate nafasi ya kunufaika na huduma na fursa zinazopatikana viwanjani hapo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Muliro Jumanne, amesema hali ya usalama katika viwanja vya Sabasaba na maeneo ya jiji inaendelea kuwa shwari, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea kuhakikisha wananchi na mali zao vinakuwa salama katika kipindi chote cha maonesho.

Baadhi ya wananchi waliotembelea maonesho hayo wameeleza kuwa uwepo wa huduma za afya, ushauri wa kisheria, elimu pamoja na bidhaa zinazouzwa kwa bei nafuu umeifanya Sabasaba 2026 kuwa zaidi ya maonesho ya biashara, bali pia kituo muhimu cha utoaji wa huduma zinazogusa maisha ya wananchi.













No comments