RAIS SAMIA AHIMIZA UWEKEZAJI VIWANDA VYA DAWA NA VIFAA TIBA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Wizara ya Afya kuharakisha juhudi za kuvutia wawekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa za afya na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Akizungumza leo Julai 1, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kumuapisha Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, Rais Samia amesema uwekezaji katika viwanda vya ndani ni nguzo muhimu ya kuimarisha sekta ya afya na kuhakikisha dawa, chanjo na vifaa tiba vinapatikana kwa urahisi.
Rais Samia amemtaka Dkt. Magembe kushirikiana na wadau mbalimbali kuwakaribisha wawekezaji wenye uwezo wa kuanzisha viwanda hivyo, huku akisisitiza uzalishaji uzingatie viwango vya ubora ili bidhaa zinazozalishwa zikidhi mahitaji ya wananchi na soko la kimataifa.
Amesema hatua hiyo itaongeza upatikanaji wa dawa na chanjo, ikiwemo chanjo za watoto, kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa kutoka nje na kuifanya Tanzania kuwa na mfumo imara wa upatikanaji wa bidhaa za afya.
Aidha, Rais Samia amemtaka Katibu Mkuu huyo mpya kutumia ipasavyo bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 ili kuhakikisha vipaumbele vya sekta ya afya vinatekelezwa kwa ufanisi na huduma kwa wananchi zinaendelea kuboreshwa.
Pia amesisitiza umuhimu wa kujenga ushirikiano mzuri na watumishi wa sekta ya afya, akieleza kuwa mafanikio ya wizara yatategemea uwezo wa viongozi kufanya kazi kwa pamoja na wataalamu wa afya.
Dkt. Grace Magembe ameapishwa kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kufuatia uteuzi wa hivi karibuni, akichukua nafasi ya Dkt. Seif Shekalaghe aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria.

Post a Comment