CP MWEN-DAD: USAHIHI NA UWAJIBIKAJI NDIO NGUZO YA MAFANIKIO YA MFUMO WA NEST
Jeshi la Magereza limekamilisha mafunzo maalum ya siku nne yaliyolenga kuwajengea uwezo maafisa na askari katika matumizi ya Mfumo mpya wa Kitaifa wa Ununuzi wa Kielektroniki (NeST), hatua inayolenga kuongeza uwazi na kudhibiti matumizi ya fedha za umma ndani ya Jeshi la Magereza.
Mafunzo hayo yamefungwa rasmi leo Septemba 24, 2026, katika Ukumbi wa Rugimbana uliopo Msalato jijini Dodoma, yamekuja wakati serikali ikihimiza taasisi zake zote za umma kuachana na mifumo ya zamani ya karatasi na kuhamia kidijitali.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu Jeshi la Magereza, CP Ahmad S. Mwendadi, amewataka washiriki kuwa watumiaji waaminifu na wenye kuwajibika wanapotumia mfumo huo mpya.
"Kila mmoja anapaswa kuhakikisha taarifa anazoingiza au kuzithibitisha katika mfumo huu ni sahihi, kamili, na zinawasilishwa kwa wakati. Hii ni muhimu katika kuhakikisha mfumo unatumika kama chombo cha kuboresha udhibiti na usimamizi wa mchakato wa ununuzi," amesisitiza CP Mwendadi.
Katika kipindi cha siku nne za mafunzo hayo, maafisa hao wamejifunza maeneo mbalimbali ya kimkakati ikiwemo uanzishaji na usimamizi wa mahitaji, upekuzi wa taarifa za mikataba, ufuatiliaji wa utekelezaji wake, pamoja na taratibu za malipo kwa njia ya kielektroniki.
CP Mwendadi ametoa shukrani za dhati kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) pamoja na wawezeshaji kutoka mamlaka hiyo, Mhandisi Damas Makweba na Ndugu Vincent Mgonja, kwa kutoa utaalamu wao uliosaidia kufanikisha mafunzo hayo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi cha Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Henry Masawe, amebainisha kuwa mafunzo hayo yamehusisha jumla ya washiriki 102 kutoka idara mbalimbali zilizopo chini ndani ya Jeshi.

Post a Comment