MAAFISA NA ASKARI MAGEREZA MKOA KILIMANJARO WAPATIWA MAFUNZO YA ELIMU YA FEDHA NA BENKI KUU
Na Wdr. Seif Baruti - KILIMANJARO
Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Kilimanjaro wamepatiwa mafunzo maalum ya elimu ya fedha na uwekezaji katika Hati Fungani za Serikali, yakilenga kuwawezesha kujipanga kifedha na kuandaa maisha bora kabla na baada ya kustaafu utumishi wao.
Mafunzo hayo yametolewa na wawezeshaji kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Tawi la Arusha, na kufanyika katika ukumbi wa Selig Annex Hotel mjini Moshi.
Akitoa mafunzo hayo, Septemba 24, 2026, Afisa Fedha Benki Kuu ya Tanzania, Yuston Mollel, amewataka maafisa na askari hao kuanza kujipanga mapema kabla ya kustaafu kwa kuweka akiba na kuwekeza katika fursa zitakazowasaidia kuendelea kuwa na utulivu wa kifedha baada ya utumishi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Leonard Burushi, amesema elimu hiyo ni muhimu kwa kuwa inawajengea uwezo wa kusimamia fedha zao na kujiandaa mapema kwa maisha ya baada ya kustaafu.
Naye Mkuu wa Gereza Kuu Karanga, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Dedan Lwemnana, ameeleza kuwa mafunzo hayo yamewapa maafisa na askari uwezo wa kuelewa namna bora ya kupanga matumizi, kuweka akiba, na kufanya uwekezaji sahihi utakaowasaidia kufanya maamuzi bora ya kifedha kwa ajili ya maisha ya baadaye.

Post a Comment