MAKONDA AAHIDI SH MILIONI 500 KUIMARISHA SHIMIWI 2027 ARUSHA



Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameahidi kutoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara na Wakala za Serikali Nchini (SHIMIWI) yatakayofanyika mwaka 2027 mkoani Arusha.

Makonda ametoa ahadi hiyo leo, Septemba 26, 2026, wakati akiwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Michezo ya 40 ya SHIMIWI uliofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi (CCP), Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Amesema mashindano ya SHIMIWI ya mwaka 2027 yatafanyika mkoani Arusha, huku akieleza kuwa fedha hizo zitatumika kuimarisha na kuboresha mashindano hayo.

Ufunguzi wa mashindano ya mwaka huu umeambatana na maandamano yaliyowakutanisha watumishi kutoka sekta mbalimbali za Serikali, hatua iliyolenga kuhamasisha mshikamano na ushirikiano miongoni mwa watumishi kupitia michezo.

SHIMIWI ni mashindano yanayowakutanisha watumishi wa Wizara, Idara na Wakala mbalimbali za Serikali katika michezo tofauti, yakilenga pia kukuza afya, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa watumishi.













No comments