RAS Kayombo, ataka maandalizi ya miundombinu ya shule za sekondari ili kupokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka 2028
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Pwani (RAS), Richard Kayombo, amesisitiza umuhimu wa kuanza mapema maandalizi ya miundombinu ya shule za sekondari kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka 2028, ambapo wanafunzi wa Darasa la Sita na la Saba wanatarajiwa kujiunga kwa pamoja kutokana na mabadiliko ya mfumo wa elimu.
Akifunga mkutano wa uchaguzi mdogo wa kumchagua Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa (KUT) wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kayombo amewahimiza walimu wenye ulemavu kutoruhusu hali hiyo kuwakatisha tamaa, huku akieleza kuwa Serikali inaendelea kushughulikia changamoto za walimu, ikiwemo ajira, upandishaji wa madaraja na malipo ya stahiki zao.
Aidha, amewaelekeza maofisa elimu kuhakikisha walimu wanatendewa haki katika upandishaji wa madaraja kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, huku akiwataka walimu kuwa mabalozi wa kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu namna ya kujikinga na kukabiliana na athari za mvua za El Niño.
Kwa upande wake, Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Suzan Shesha, amesema mkoa huo una jumla ya walimu 11,000, akimuomba RAS kusimamia uendeshaji wa mabaraza ya wafanyakazi kwa wakati ili kuimarisha mawasiliano na utatuzi wa kero za walimu.
Katika uchaguzi huo, Mwita Magige ameshinda nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa kwa kupata kura 20, dhidi ya Abdalrahmani Ahmadi aliyepata kura 16, huku kura moja ikiharibika kati ya kura 37 zilizopigwa.


.jpeg)
.jpeg)


Post a Comment