WATAALAMU wa afya wahimizwa kuimarisha juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya ugonjwa wa malaria

 


WATAALAMU wa afya wamehimiza kuimarishwa kwa juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya ugonjwa wa malaria, wakieleza kuwa maambukizi yanayojirudia yanaweza kuathiri ukuaji wao, maendeleo ya kielimu na ustawi wa familia, hali inayoweza kudhoofisha uwezo wa kizazi kijacho kuchangia maendeleo ya Afrika.


Mwanasayansi Kiongozi wa Mradi wa Transmission Zero katika Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Daktari Brian Tarimo, amesema malaria haiathiri afya ya mtoto pekee anapougua, bali pia huathiri mchakato wa kujifunza, utulivu wa familia na uwezo wa vijana kufikia malengo yao.


Amesema kila mtoto anastahili kupata fursa ya kukua, kujifunza na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii bila kukumbwa na athari za magonjwa yanayoweza kuzuilika, yakiwemo maambukizi ya malaria yanayojirudia.


Dkt. Tarimo ameeleza kuwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kuugua malaria barani Afrika, huku familia zenye watoto wanaougua mara kwa mara zikikabiliwa na changamoto za kimwili, kihisia na kiuchumi.



Katika kukabiliana na ugonjwa huo, Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kwa kushirikiana na Imperial College London na Swiss Tropical and Public Health Institute, zinaendeleza tafiti za teknolojia ya kijenetiki inayojulikana kama gene drive kupitia Mradi wa Transmission Zero.


Teknolojia hiyo inalenga kuwezesha sifa maalumu za kijenetiki kurithishwa kwa kiwango kikubwa zaidi katika mbu, kwa lengo la kuwafanya mbu wanaosambaza malaria washindwe kusambaza vimelea vya ugonjwa huo kwa binadamu.






No comments